4. Mwingine ni mfalme Ogu mmoja wa Warefai waliosalia, ambaye alitawala Bashani na alikaa Ashtarothi au Edrei.
5. Utawala wake ulienea huko kwenye mlima Hermoni, huko Saleka, Bashani yote mpaka mipaka ya Wageshuri na Wamaaka, nusu ya Gileadi hadi mpakani mwa nchi ya mfalme Sihoni wa Heshboni.
6. Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, pamoja na Waisraeli aliwashinda wafalme hao, akayapatia nchi hizo makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase ziwe mali yao kabisa.
7. Kisha Yoshua pamoja na Waisraeli waliwashinda wafalme wote wa eneo lote lililoko magharibi ya mto Yordani, kuanzia Baal-gadi katika bonde la Lebanoni mpaka mlima uliokuwa mtupu wa Halaki kusini karibu na Seiri. Yoshua akayagawia makabila ya Israeli nchi hizo ziwe mali yao kabisa.
8. Nchi hizo zilikuwa pamoja na maeneo ya milima, nchi tambarare, eneo la Araba, miteremko ya milima, maeneo ya nyika, na eneo la Negebu; nchi zilizokuwa za Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi.