21. Baada ya hayo Waisraeli wote walirudi salama kwa Yoshua huko kambini Makeda; na hakuna tena mtu aliyethubutu kusema lolote dhidi ya Waisraeli.
22. Kisha Yoshua akasema, “Fungueni mlango wa pango mniletee kutoka humo wale wafalme watano.”
23. Wakafanya hivyo, wakamletea Yoshua wale wafalme watano: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni.
24. Wafalme hao walipoletwa, Yoshua akawaita Waisraeli wote na wakuu wa majeshi waliokwenda naye vitani, akawaambia, “Njoni karibu mwakanyage wafalme hawa shingoni mwao.” Nao wakasogea na kuwakanyaga shingoni.
25. Yoshua akawaambia “Msiogope, wala msiwe na wasiwasi, muwe imara na hodari, maana hivi ndivyo Mwenyezi-Mungu atakavyowatendea adui zenu ambao mtapigana nao. Kwa hiyo, muwe imara na hodari.”
26. Baadaye, Yoshua aliwanyonga kwa kuwaangika kwenye miti mitano ambako walitundikwa mpaka jioni.
27. Wakati jua lilipokuwa karibu kutua, Yoshua aliamuru waondolewe juu ya miti walipokuwa wameangikwa na kutupwa pangoni walimokuwa wamejificha. Kisha wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, nayo mawe hayo yako huko mpaka leo.
28. Siku hiyo Yoshua alipouteka mji wa Makeda, alimuua mfalme wake na wakazi wake wote bila kumbakiza hata mtu mmoja. Alimtendea mfalme wa Makeda kama vile alivyomtendea mfalme wa Yeriko.
29. Kutoka Makeda, Yoshua pamoja na Waisraeli wote walikwenda Libna wakaushambulia.