37. Najua kwamba nyinyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamyakubali mafundisho yangu.
38. Mimi nasema yale aliyonionesha Baba, lakini nyinyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu.”
39. Wao wakamjibu, “Sisi ni watoto wa Abrahamu!” Yesu akawaambia, “Kama nyinyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu.
40. Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, nyinyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo!
41. Nyinyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya baba yenu.” Wao wakamwambia, “Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu.”
42. Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
43. Kwa nini hamuelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu.