Yobu 36:17-29 Biblia Habari Njema (BHN)

17. “Lakini sasa umehukumiwa kama mwovu,hukumu ya haki imekukumba.

18. Jihadhari ghadhabu isije ikakufanya ukadhihaki,au ukubwa wa mali za kukukomboa ukakupotosha.

19. Je, kilio chako kitafaa kukutoa taabuni,au nguvu zako zote zitakusaidia?

20. Usitamani usiku uje,ambapo watu hufanywa watoweke walipo.

21. Jihadhari! Usiuelekee uovumaana umepatiwa mateso kukuepusha na uovu.

22. Kumbuka ukuu wa uwezo wa Mungu;nani awezaye kumfundisha kitu?

23. Nani basi aliyeweza kumpangia njia yake,au awezaye kumwambia: ‘Umekosea?’

24. “Usisahau kuyasifu matendo yake;ambayo watu wameyashangilia.

25. Watu wote wameona aliyofanya Mungu;binadamu huyaona kutoka mbali.

26. Mungu ni mkuu mno hata hatuwezi kumjua;muda wa maisha yake hauchunguziki.

27. Yeye huyavuta kwake maji ya bahari,na kutoka ukungu hufanya matone ya mvua.

28. Huyafanya mawingu yanyeshe mvua,na kuwatiririshia binadamu kwa wingi.

29. Nani ajuaye jinsi mawingu yatandavyo,au jinsi radi ingurumavyo angani kwake?

Yobu 36