Yeremia 49:19-38 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Kama vile simba anavyochomoza kutoka msitu wa mto Yordani na kuingia kwenye malisho mazuri, ndivyo nitakavyowafukuza ghafla Waedomu kutoka nchi yao. Nami nitamweka huko kiongozi yeyote nitakayemchagua. Maana, ni nani anayeweza kulinganishwa nami? Nani awezaye kunishtaki? Ni mchungaji gani awezaye kunipinga?

20. Kwa hiyo, sikilizeni mpango ambao mimi Mwenyezi-Mungu nimepanga dhidi ya Edomu pamoja na mambo niliyokusudia kuwafanyia wakazi wa Temani: Hakika, watoto wao wadogo wataburutwa na kuchukuliwa; kweli kutakuwa na mshangao mkubwa katika makao yao!

21. Kwa kishindo cha kuanguka kwao, dunia itatetemeka; sauti ya kilio chao itasikika mpaka bahari ya Shamu.

22. Tazama, adui atapanda juu na kuruka kama tai na kutandaza mabawa yake juu ya Bosra. Siku hiyo moyo wa mashujaa wa Edomu utakumbwa na hofu kama ya mwanamke anayejifungua.”

23. Kuhusu Damasko:“Miji ya Hamathi na Arpadi, imejaa wasiwasikwa kufikiwa na habari mbaya;mioyo ya watu wake inayeyuka kwa hofu,imefadhaika kama bahari isiyoweza kutulia.

24. Watu wa Damasko wamekufa moyo;wamegeuka wapate kukimbia;hofu kubwa imewakumba,uchungu na huzuni vimewapata,kama mwanamke anayejifungua

25. Ajabu kuachwa kwa mji maarufu,mji uliokuwa umejaa furaha!

26. Basi vijana wake wataanguka viwanjani mwake,askari wake wote wataangamizwa siku hiyo.Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimesema.

27. Nitawasha moto katika kuta za Damasko,nao utateketeza ngome za mfalme Ben-hadadi.”

28. Kuhusu Kedari na falme za Hazori ambazo Nebukadneza mfalme wa Babuloni, alizishambulia na kuzishinda, Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Inuka uende kulishambulia kabila la Kedari!Waangamize watu wa mashariki!

29. Hema zao na kondoo wao vitachukuliwa,kadhalika mapazia yao na mali yao yote;watanyanganywa ngamia wao,na kilio kitasikika: ‘Kitisho kila upande!’

30. Kimbieni, nendeni mbali, kaeni mashimoni.Enyi wakazi wa Haziri,kimbieni mtangetange na kukaa mafichoni!Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.Maana Nebukadneza mfalme wa Babuloni,amefanya mpango dhidi yenu,amepania kuja kuwashambulia.

31. Inuka uende kulishambulia taifa linalostarehe,taifa linaloishi kwa usalama.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.Taifa hilo halina malango wala pao za chuma;ni taifa ambalo liko peke yake.

32. “Ngamia wao watatekwamifugo yao itachukuliwa mateka.Nitawatawanya kila upande,watu wale wanaonyoa denge.Nitawaletea maafa kutoka kila upande.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

33. Mji wa Hazori utakuwa makao ya mbweha,utakuwa jangwa daima;hakuna mtu atakayekaa humo,wala atakayeishi humo.”

34. Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Elamu, mwanzoni mwa utawala wa Sedekia, mfalme wa Yuda.

35. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, asema hivi: “Nitavunja upinde wa watu wa Elamu ulio msingi wa nguvu zao.

36. Nitaleta upepo kutoka pande zote za mbingu; nitawatawanya kila mahali, wala hapatakuwa na taifa lolote ambalo halitakuwa na wakimbizi wa Elamu.

37. Nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya maadui zao na mbele ya wale wanaotaka kuyaangamiza maisha yao. Nitawaletea maafa na hasira yangu kali. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitawaletea upanga kuwafuata mpaka niwaangamize kabisa.

38. Nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu na kumwangamiza mfalme wao pamoja na wakuu wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

Yeremia 49