32. Naam, mimi Mwenyezi-Mungu nasema kuwa nitawashambulia manabii wanaotabiri ndoto zao za uongo kwa watu wangu, na kuwapotosha kwa uongo wao na kuropoka kwao. Mimi sikuwatuma wala kuwaamuru waende; kwa hiyo hawatawafaa watu hao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
33. Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Mtu yeyote, awe nabii au kuhani, akikuuliza: ‘Uko wapi mzigo anaotubebesha Mwenyezi-Mungu?’ Wewe utawaambia: ‘Nyinyi ndio mzigo kwa Mwenyezi-Mungu naye atawatupa mbali.’
34. Tena nabii au kuhani, au mtu yeyote atakayesema ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ nitamwadhibu pamoja na jamaa yake yote.
35. Kitu mnachopaswa kuulizana nyinyi kwa nyinyi ni ‘Mwenyezi-Mungu amejibu nini?’ au, ‘Mwenyezi-Mungu amesema nini?’
36. Lakini jambo la ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ msilitaje tena. Kile anachosema binadamu ni mzigo kwake mwenyewe. Watu wanayapotosha maneno ya Mungu aliye hai, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wao.
37. Basi mtamwuliza nabii hivi: ‘Mwenyezi-Mungu amekujibu nini?’ au, ‘Mwenyezi-Mungu amesema nini?’
38. Lakini wao wakivunja amri yangu na kusema, ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ wakati ambapo mimi niliwakataza wasiseme, ‘Mzigo wa Mwenyezi-Mungu,’ basi, waambie kuwa
39. mimi nitawanyanyua na kuwatupilia mbali, wao wenyewe pamoja na mji niliowapa wao na wazee wao.
40. Nitawaletea fedheha ya milele na aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.”