Walawi 8:25-32 Biblia Habari Njema (BHN)

25. Kisha, akachukua mafuta yote, mkia pamoja na mafuta yake, mafuta yote yanayofunika matumbo, sehemu bora ya ini, pamoja na figo zote mbili, mafuta yake na paja la mguu wa kulia wa nyuma wa huyo kondoo dume.

26. Kisha, kwenye kile kikapu cha mikate iliyowekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu akatoa mkate mmoja usiotiwa chachu, mkate mmoja wenye mafuta na mkate mmoja mdogo, akaviweka vyote juu ya vipande vya mafuta na ule mguu.

27. Mose akaviweka mikononi mwao Aroni na wanawe, nao wakafanya ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu.

28. Kisha Mose akavichukua vitu hivyo vyote kutoka mikononi mwao na kuviteketeza juu ya madhabahu pamoja na sadaka ya kuteketezwa. Hii ni sadaka ya kuwekwa wakfu, yenye harufu ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu; ni sadaka itolewayo kwa moto.

29. Kisha Mose akachukua kile kidari na kufanya ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu. Sehemu hiyo ya yule kondoo dume wa kuweka wakfu ni mali yake Mose kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.

30. Halafu Mose akachukua mafuta ya kupaka na damu kutoka madhabahu akamnyunyizia Aroni na wanawe hata na pia mavazi yao. Hivyo Mose akamweka wakfu Aroni na wanawe pamoja na mavazi yao.

31. Mose akamwambia Aroni na wanawe, “Chemsheni ile nyama mbele ya mlango wa hema la mkutano, muile hapo mlangoni pamoja na mkate kutoka katika kikapu chenye sadaka za kuwekea wakfu. Fanyeni kama nilivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, kwamba sehemu hiyo italiwa na Aroni na wanawe.

32. Nyama yoyote au mkate wowote utakaosalia ni lazima kuteketezwa.

Walawi 8