6. Kisha atamletea kuhani kondoo dume au mbuzi dume asiye na dosari amtolee Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuondoa hatia; thamani ya mnyama huyo itakuwa ile ya kawaida ya kuondoa hatia.
7. Kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye atasamehewa kosa ambalo alikuwa amelifanya.”
8. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
9. “Mpe Aroni na wanawe maagizo haya: Ufuatao ni mwongozo wa ibada kuhusu sadaka ya kuteketezwa. Sadaka ya kuteketezwa itakuwa motoni juu ya madhabahu usiku kucha hadi asubuhi na moto wake uchochewe, usizimike.
10. Kisha kuhani akiwa amevaa vazi lake rasmi la kitani na kaptura yake ya kitani, atachukua majivu ya ile sadaka kutoka madhabahuni na kuyaweka kando ya madhabahu.
11. Halafu baada ya kubadilisha mavazi yake atayapeleka yale majivu nje ya kambi mahali palipo safi.
12. Moto wa madhabahu lazima uendelee kuwaka, na wala usizimwe. Kila siku asubuhi kuhani ataweka kuni kwenye moto huo na juu yake atapanga sadaka ya kuteketezwa, kabla ya kuteketeza mafuta ya sadaka ya amani.