Walawi 23:38-44 Biblia Habari Njema (BHN)

38. Sadaka hizo ni pamoja na zile mnazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu siku ya Sabato kama vile pia sadaka zenu za kawaida, sadaka za kutimiza nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari mnazonitolea mimi Mwenyezi-Mungu.

39. “Baada ya kuvuna mashamba yenu mtafanya sikukuu kwa muda wa siku saba, tangu siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba. Siku ya kwanza itakuwa siku ya mapumziko na hata siku ya nane.

40. Katika siku ya kwanza mtachukua matunda ya miti yenu mizuri, matawi ya mitende, matawi yenye majani mengi na matawi ya miti iotayo kandokando ya mto, nanyi mtafanya sherehe mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kwa siku saba.

41. Kila mwaka ni lazima kuadhimisha sikukuu hii kwa muda wa siku saba kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu. Mtaifanya katika mwezi wa saba.

42. Kwa muda wa siku saba mtaishi katika vibanda. Wakazi wote wa Israeli wataishi katika vibanda wakati huo.

43. Jambo hilo litavijulisha vizazi vyenu kuwa nilipowatoa babu zenu nchini Misri, niliwafanya waishi katika vibanda. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”

44. Mose akawatangazia Waisraeli sikukuu za Mwenyezi-Mungu zilizopangwa.

Walawi 23