14. Kabla ya siku hiyo ya kuniletea mimi Mungu wenu sadaka hiyo, hamruhusiwi kula mazao ya kwanza ya mavuno yenu, yawe mabichi, yamekaangwa au yemeokwa kuwa mikate. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu mahali popote mtakapoishi.
15. “Mtahesabu majuma saba kamili tangu siku ile inayofuata Sabato ile ambapo mtaleta mganda wa sadaka ya kunitolea kwa ishara mimi Mwenyezi-Mungu.
16. Mnamo siku ya hamsini, siku ya pili ya Sabato ya saba, mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka ya nafaka mpya.
17. Kila jamaa italeta mikate miwili ya sadaka ya kutoa kwa ishara mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu. Kila mkate ni lazima uwe umetengenezwa kwa kilo mbili za unga laini uliotiwa chachu; na huo mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu ukiwa ni matoleo ya malimbuko yenu.
18. Pamoja na hayo, mtatoa wanakondoo saba wa mwaka mmoja, fahali mchanga mmoja, na kondoo madume wawili. Wanyama hao watakuwa sadaka ya kuteketezwa pamoja na sadaka ya nafaka na sadaka za kinywaji. Harufu ya sadaka hizi itanipendeza mimi Mwenyezi-Mungu.
19. Mtatoa beberu mmoja wa sadaka ya kuondoa dhambi na wanakondoo madume wawili wa mwaka mmoja kwa ajili ya sadaka za amani.
20. Kuhani atavipitisha mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu viwe sadaka ya kutoa kwa ishara pamoja na mkate wa mavuno ya kwanza na wale wanakondoo wawili. Vitu hivyo ni vitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu navyo vitakuwa kwa matumizi ya kuhani tu.