Walawi 21:9-17 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Binti wa kuhani yeyote akijitia unajisi kwa kufanya ukahaba, atateketezwa kwa moto kwani anamtia baba yake unajisi.

10. “Kuhani mkuu yeyote, kwa kuwa yeye ni mkuu kati ya ndugu zake, naye amemiminiwa mafuta ya kupaka kichwani pake, na kuwekwa wakfu ili ayavae mavazi matakatifu, asiache nywele zake kuwa ovyo wala asirarue mavazi yake kuomboleza.

11. Asikaribie maiti wala kujitia unajisi kwa maiti hata kama ni ya baba yake au ya mama yake.

12. Kwa kuwa amewekwa wakfu kwa kupakwa mafuta ya Mungu wake kichwani, basi asiondoke mahali patakatifu wala asipatie unajisi. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

13. Kuhani mkuu aweza tu kumwoa msichana ambaye ni bikira.

14. Haruhusiwi kuoa mwanamke mjane, mwanamke asiye bikira, wala kahaba. Ni lazima aoe bikira kutoka watu wake mwenyewe

15. asije akawatia unajisi watoto wake mwenyewe. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu niliyemweka wakfu.”

16. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,

17. “Mwambie Aroni hivi: Mzawa wako yeyote katika vizazi vyote vijavyo ambaye ana dosari mwilini, haruhusiwi kukaribia na kunitolea mimi Mungu wake sadaka ya mkate.

Walawi 21