Walawi 14:48-57 Biblia Habari Njema (BHN)

48. “Lakini ikiwa baada ya kuikagua nyumba hiyo, kuhani ataona kuwa upele haujaenea baada ya kupigwa lipu, basi, kuhani atatangaza kuwa nyumba hiyo ni safi kwani upele umekwisha.

49. Ili kuitakasa nyumba hiyo, mwenye nyumba ataleta ndege wawili pamoja na kipande cha mwerezi, sufu nyekundu na tawi la husopo.

50. Atamchinja ndege mmoja katika chungu chenye maji safi ya chemchemi.

51. Atachukua kipande cha mwerezi, tawi la husopo na ile sufu nyekundu pamoja na yule ndege mwingine aliye hai na kuvitumbukiza vyote katika damu ya yule ndege aliyechinjwa. Kisha atainyunyizia nyumba hiyo damu mara saba.

52. Hivyo ndivyo atakavyoitakasa nyumba hiyo kwa damu ya ndege, maji safi ya chemchemi, ndege hai, kipande cha mwerezi, tawi la husopo na ile sufu nyekundu.

53. Yule ndege hai atamwacha aende zake mashambani nje ya mji. Hivyo ndivyo atakavyoitakasa nyumba hiyo, nayo itakuwa safi.”

54. Hii ndiyo sheria kuhusu aina yoyote ya namna ya upele wa ukoma;

55. upele katika nguo au nyumba,

56. uvimbe, jipu au kipaku,

57. ili kuonesha ni kitu gani kilicho najisi na kisicho najisi. Hiyo ndiyo sheria kuhusu namna ya upele wa ukoma.

Walawi 14