15. Hivyo yeye ni mpatanishi wa agano jipya ambamo wale walioitwa na Mungu wanaweza kupokea baraka za milele walizoahidiwa. Kifo chake huwakomboa watu kutoka yale makosa waliyofanya wakati wa lile agano la kale.
16. Kwa kawaida wosia hutambuliwa tu kama kifo cha yule aliyeufanya huo wosia kimethibitishwa.
17. Wosia hauwezi kutekelezwa mpaka kumetokea kifo, kwani wosia hauna maana ikiwa mwenye kuufanya bado anaishi.
18. Ndiyo maana hata lile agano la kwanza halikuwekwa bila damu kumwagwa.
19. Kwanza Mose aliwatangazia watu wote amri zote kama ilivyokuwa katika sheria; kisha akachukua damu ya ndama pamoja na maji, na kwa majani ya mti wa husopo na pamba nyekundu, akakinyunyizia kile kitabu cha sheria na watu wote.
20. Mose alisema: “Hii ni damu inayothibitisha agano mliloamriwa na Mungu mlitii.”