28. Kwa imani aliadhimisha siku ya Pasaka, akaamuru damu inyunyizwe juu ya milango, ili yule Malaika Mwangamizi asiwaue wazaliwa wa kwanza wa Israeli.
29. Kwa imani watu wa Israeli walivuka bahari ya Shamu kana kwamba ilikuwa nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo walikufa maji.
30. Kwa imani kuta za mji wa Yeriko zilianguka watu wa Israeli walipokwisha zunguka kuta hizo kwa siku saba.
31. Kwa imani Rahabu aliyekuwa malaya hakuangamia pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa sababu aliwakaribisha wale wapelelezi.
32. Basi, niseme nini zaidi? Wakati hauniruhusu kueleza juu ya Gideoni, Baraki, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samueli na manabii.
33. Kwa imani hawa wote walipigana vita na wafalme, wakashinda. Walitenda mambo adili, wakapokea yale aliyoahidi Mungu. Walifunga vinywa vya simba,
34. walizima mioto mikali, waliepuka kuuawa kwa upanga, walikuwa dhaifu lakini walipata nguvu. Walikuwa hodari katika vita, wakashinda majeshi ya kigeni.