Waamuzi 8:3-9 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Mungu amewatia mikononi mwenu wakuu wa Midiani, Orebu, na Zeebu. Je, mimi nimefanya nini nikilinganishwa nanyi?” Gideoni alipokwisha sema hivyo, hasira yao dhidi yake ikatulia.

4. Gideoni na wenzake 300 wakafika Yordani, wakavuka. Ingawa walikuwa wamechoka sana, waliendelea kuwafuatia adui zao.

5. Basi, akawaambia watu wa Sukothi, “Tafadhali wapeni wenzangu hawa mikate maana wamechoka sana; nami bado ninaendelea kuwafuatia wafalme Zeba na Salmuna wa Midiani.”

6. Lakini viongozi wa Sukothi wakamwuliza, “Kwa nini tuwape mikate nanyi bado hamjamshinda Zeba na Salmuna?”

7. Gideoni akawaambia, “Sawa, lakini Mwenyezi-Mungu atakapowatia Zeba na Salmuna mikononi mwangu, nitaichanachana miili yenu kwa miiba na mbigili za jangwani.”

8. Kutoka huko akawaendea watu wa Penueli, akawaomba namna ileile. Nao watu wa Penueli wakamjibu kama walivyomjibu watu wa Sukothi.

9. Gideoni akawaambia, “Nitakaporudi kwa amani nitaubomoa mnara huu.”

Waamuzi 8