31. Kisha watu wa kabila la Benyamini walipotoka mjini kuanza kupigana na Waisraeli, walivutwa kutoka nje ya mji. Ilitokea tena kama walivyofanya nyakati za hapo awali wakawaua baadhi ya watu wa Israeli kwenye njia kuu zielekeazo miji ya Betheli na Gibea, mpaka mbugani. Waliua Waisraeli wapatao thelathini.
32. Watu wa Benyamini wakafikiri, “Tumewapiga kama nyakati zilizopita.” Lakini Waisraeli wakasema, “Sisi tukimbie ili tuwavute mbali na mji hadi kwenye njia kuu.”
33. Hivyo watu wote wa Israeli wakatoka kwenye sehemu yao na kujipanga tena huko Baal-tamari. Wenzao waliokuwa wanaotea wakatoka haraka mahali pao upande wa magharibi wa mji wa Gibea.
34. Askari hodari waliochaguliwa kutoka makabila yote ya Israeli wakawasili hapo mbele ya mji wa Gibea. Vita vya siku hiyo vilikuwa vikali. Lakini watu wa Benyamini hawakufahamu kwamba kuangamia kwao kulikuwa karibu.
35. Mwenyezi-Mungu aliwashinda watu wa Benyamini mbele ya Waisraeli. Waisraeli wakawaua watu wa Benyamini 25,100. Hao wote waliouawa walikuwa askari walioweza kutumia silaha.