1. Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja, akaniambia, “Njoo, nami nitakuonesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu, mji ule uliojengwa juu ya maji mengi.
2. Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi wa dunia wamelewa divai ya uzinzi wake.”
3. Kisha, nikakumbwa na Roho mpaka jangwani. Huko nikamwona mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa ameandikwa kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.
4. Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu. Mkononi mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa machukizo na mambo machafu yanayoonesha uzinzi wake.
5. Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo “Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana duniani.”
6. Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya watu waliouawa kwa sababu ya kumshuhudia Yesu.Nilipomwona nilishangaa mno.
7. Lakini malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Mimi nitakuambia maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye ambaye ana vichwa saba na pembe kumi.
8. Huyo mnyama uliyemwona, alikuwa hai hapo awali lakini sasa amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao majina yao hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uhai tangu mwanzo wa ulimwengu, watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali aliishi, kisha akafa na sasa anatokea tena!