Mwanzo 48:4-12 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Aliniambia, ‘Tazama, nitakufanya uwe na wazawa na uongezeke; nitakufanya uwe babu wa jamii kubwa za watu. Ardhi hii nitawapa wazawa wako, waimiliki milele.’”

5. Yakobo akaendelea kusema, “Wanao wawili uliowapata hapa Misri kabla sijafika, ni wanangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu kama walivyo Reubeni na Simeoni.

6. Lakini, watoto utakaopata baadaye watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao.

7. Naamua hivyo kwa sababu ya mama yako, Raheli. Nilipokuwa narudi kutoka Padani yeye alifariki katika nchi ya Kanaani, tukiwa karibu kufika Efratha, akaniachia huzuni. Basi, nikamzika papo hapo, kando ya njia iendayo Efratha, yaani Bethlehemu.”

8. Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akamwuliza, “Ni akina nani hawa?”

9. Yosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wanangu alionijalia Mungu nikiwa huku.” Israeli akasema, “Tafadhali, walete karibu nipate kuwabariki.”

10. Macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee. Basi, Yosefu akawasogeza wanawe karibu na baba yake, naye akawabusu na kuwakumbatia.

11. Kisha Israeli akamwambia Yosefu, “Sikutazamia kuuona uso wako tena; lakini, kumbe, Mungu amenijalia hata kuwaona watoto wako!”

12. Hapo Yosefu akawaondoa wanawe kwenye magoti ya baba yake, kisha akainama kwa heshima.

Mwanzo 48