Mwanzo 37:3-12 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Israeli alimpenda Yosefu kuliko watoto wake wote kwa sababu alikuwa amezaliwa wakati wa uzee wake. Alimshonea Yosefu kanzu ndefu.

4. Lakini ndugu zake walipoona kwamba baba yao alimpenda Yosefu kuliko wao, wakamchukia hata hawakuzungumza naye kwa amani.

5. Usiku mmoja, Yosefu aliota ndoto, lakini alipowasimulia ndugu zake, wao wakazidi kumchukia.

6. Aliwaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota:

7. Niliota kuwa sote tulikuwa shambani tukifunga miganda na ghafla mganda wangu ukainuka na kusimama wima. Miganda yenu ikakusanyika kuuzunguka na kuuinamia mganda wangu.”

8. Ndugu zake wakamwuliza, “Je, unataka kutuambia kwamba utatutawala? Au utakuwa na mamlaka juu yetu?” Basi, wakazidi kumchukia kwa sababu ya ndoto na maneno yake.

9. Kisha Yosefu akaota ndoto nyingine, akawasimulia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine; nimeona jua, mwezi na nyota kumi na moja vinaniinamia.”

10. Lakini alipomsimulia baba yake na ndugu zake ndoto hiyo, baba yake alimkemea akisema, “Ni ndoto gani hiyo uliyoota? Je, itatulazimu mimi, mama yako na ndugu zako kuja kuinama chini kwa heshima mbele yako?”

11. Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akawa analifikiria jambo hilo.

12. Siku moja, ndugu zake Yosefu walikwenda kuchunga wanyama wa baba yao karibu na Shekemu.

Mwanzo 37