15. Lakini Lea akamsemea kwa ukali, “Je, unadhani ni jambo dogo kuninyanganya mume wangu, na sasa unataka kuchukua tunguja za mwanangu?” Raheli akamjibu, “Ikiwa utanipa tunguja za mwanao, Yakobo atalala kwako leo.”
16. Basi, jioni Yakobo alipokuwa anarudi toka shambani, Lea alitoka kwenda kumlaki, akamwambia, “Leo huna budi kulala nami, kwani nimekuajiri kwa tunguja za mwanangu.” Hivyo Yakobo akalala kwa Lea usiku huo.
17. Mungu akasikiliza ombi la Lea, naye akapata mimba na kumzalia Yakobo mtoto wa tano wa kiume.
18. Lea akasema, “Mungu amenipa ujira wangu kwa sababu nilimpa mume wangu mjakazi wangu.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Isakari.
19. Lea akapata mimba tena na kumzalia Yakobo mtoto wa sita wa kiume.
20. Akasema, “Mungu amenipa zawadi bora. Sasa mume wangu ataniheshimu kwa maana nimemzalia watoto sita wa kiume.” Kwa hiyo akamwita mtoto huyo Zebuluni.
21. Baadaye akazaa mtoto wa kike, akamwita Dina.