1. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Mika, mwenyeji wa Moreshethi, wakati Yothamu, Ahazi na Hezekia walipokuwa wafalme wa Yuda. Mika aliona mambo yote haya kuhusu Samaria na Yerusalemu.
2. Sikilizeni enyi watu wote;sikiliza ewe dunia na vyote vilivyomo.Mwenyezi-Mungu anakuja kuwashtaki,Bwana anena kutoka hekalu lake takatifu.
3. Naam! Mwenyezi-Mungu yuaja kutoka makao yake;atashuka na kutembea juu ya vilele vya dunia.
4. Milima itayeyuka chini ya nyayo zake,kama nta karibu na moto;mabonde yatapasuka,kama maji yaporomokayo kwenye mteremko.
5. Haya yote yatatukiakwa sababu ya makosa ya wazawa wa Yakobo,kwa sababu ya dhambi za wazawa wa Israeli.Je, uhalifu wa Yakobo waonekana wapi?Katika mji wake mkuu Samaria!Je, uhalifu wa Yuda waonekana wapi?Katika Yerusalemu kwenyewe!