Methali 16:4-19 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Mwenyezi-Mungu ameumba kila kitu kwa kusudi lake;hata waovu kwa ajili ya siku ya maangamizi.

5. Kila mwenye kiburi ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu;hakika mtu wa namna hiyo hataacha kuadhibiwa.

6. Kwa utii na uaminifu mtu huondolewa dhambi,kwa kumcha Mwenyezi-Mungu huepuka uovu.

7. Mwenyezi-Mungu akipendezwa na mwenendo wa mtu,huwageuza hata adui zake kuwa marafiki.

8. Afadhali mali kidogo kwa uadilifu,kuliko mapato mengi kwa udhalimu.

9. Mtu aweza kufanya mipango yake,lakini Mwenyezi-Mungu huongoza hatua zake.

10. Mfalme huamua kwa maongozi ya Mungu;anapotoa hukumu hakosei.

11. Mwenyezi-Mungu hutaka kipimo na mizani halali;mawe yote mfukoni ya kupimia ni kazi yake.

12. Ni chukizo kubwa wafalme kutenda uovu,maana msingi wa mamlaka yao ni haki.

13. Mfalme hupendelea mtu asemaye kwa unyofu;humpenda mtu asemaye ukweli.

14. Hasira ya mfalme ni kama mjumbe wa kifo;mtu mwenye busara ataituliza.

15. Uso wa mfalme ukingaa kuna uhai;wema wake ni kama wingu la masika.

16. Kupata hekima ni bora kuliko dhahabu;kupata akili ni chaguo bora kuliko fedha.

17. Njia ya wanyofu huepukana na uovu;anayechunga njia yake huhifadhi maisha yake.

18. Kiburi hutangulia maangamizi;majivuno hutangulia maanguko.

19. Afadhali kuwa mnyenyekevu na kuwa maskini,kuliko kugawana nyara na wenye kiburi.

Methali 16