Mathayo 25:31-43 Biblia Habari Njema (BHN)

31. “Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu.

32. Mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi.

33. Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto.

34. “Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, ‘Njoni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

35. Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha;

36. nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.’

37. Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme ‘Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji?

38. Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika?

39. Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?’

40. Mfalme atawajibu, ‘Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.’

41. “Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, ‘Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake.

42. Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji.

43. Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama.’

Mathayo 25