4. Hivyo, tambiko za watu wa Yuda na wa Yerusalemu zitampendeza Mwenyezi-Mungu kama za watu wa kale; kama katika miaka ya zamani.
5. Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema: “Kisha nitawakaribia ili kuwahukumu. Sitasita kutoa ushahidi dhidi ya wachawi, wazinzi, watoa ushahidi wa uongo, wanaowapunja waajiriwa, wanaowadhulumu wageni na wale wasionicha mimi.
6. “Mimi ni Mwenyezi-Mungu, mimi sibadiliki. Lakini nyinyi, nyinyi wazawa wa Yakobo hamjatoweka bado.
7. Tangu wakati wa wazee wenu, mmezidharau kanuni zangu wala hamkuzifuata. Basi, mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu nasema: Nirudieni, nami nitawageukieni. Lakini nyinyi mnauliza, ‘Tutakurudia namna gani?’ Nami nawaulizeni,
8. Je, ni sawa mtu kumdanganya Mungu? La! Lakini nyinyi mnanidanganya! Walakini nyinyi mwauliza: ‘Tunakudanganya kwa namna gani?’ Naam! Mnanidanganya kuhusu zaka na tambiko zenu.
9. Nyinyi na taifa lenu lote mmelaaniwa kwa sababu ya kunidanganya.