1. Kauli ya Mwenyezi-Mungu iliyomjia Malaki awaambie Waisraeli.
2. Mwenyezi-Mungu asema: “Daima nimewapenda nyinyi”. Lakini watu wa Israeli wanauliza, “Umetupendaje?” Naye Mwenyezi-Mungu asema: “Je, Esau hakuwa ndugu yake Yakobo? Hata hivyo nilimpenda Yakobo
3. nikamchukia Esau. Nimeiharibu nchi ya milima ya Esau ambayo ni urithi wake, nikawaachia mbwamwitu wa jangwani. Nao wazawa
4. wa Esau, yaani Waedomu, wanasema kwamba ingawa miji yao imeharibiwa, watajenga upya magofu yake. Lakini, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema kwamba wanaweza kuijenga upya, lakini mimi nitaibomolea mbali. Watu watawaita, ‘Taifa ovu ambalo Mwenyezi-Mungu amelikasirikia milele.’
5. Nanyi mtakapoyaona hayo kwa macho yenu, mtatambua na kusema: ‘Ukuu wa Mwenyezi-Mungu wafika hata nje ya mipaka ya nchi ya Israeli.’”
6. Mwenyezi-Mungu wa majeshi anawaambia hivi nyinyi makuhani mnaolidharau jina lake: “Mtoto humheshimu mzazi wake, na mtumishi humheshimu bwana wake. Ikiwa mimi ndiye Baba yenu, mbona mwanivunjia heshima? Ikiwa mimi ni bwana wenu, mbona hamniheshimu? Nanyi mnauliza, ‘Sisi tumekudharauje?’
7. Mwanidharau kwa kunitolea madhabahuni pangu tambiko ya chakula najisi. Lakini nyinyi mnauliza, ‘Tumekitiaje najisi?’ Mnakitia najisi kwa kuidharau madhabahu yangu.