30. Kwenye kifuko hicho utatia mawe ya kauli yaninginie kifuani mwa Aroni kila anapokuja mbele yangu. Nyakati hizo ni lazima kila mara kuvaa kifuko hicho, ili aweze kutambua matakwa yangu kuhusu Waisraeli.
31. “Utashona kanzu ya kuvalia kizibao kwa sufu ya rangi ya buluu.
32. Itakuwa na nafasi ya kupitishia kichwa katikati, na nafasi hiyo itazungushiwa utepe uliofumwa ili isichanike.
33. Kwenye upindo wake wa chini, kuzunguka pande zote, itapambwa kwa makomamanga ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, kutakuwa pia na njuga za dhahabu kati ya hayo makomamanga:
34. Komamanga, njuga, komamanga, njuga, kuizunguka kanzu yote.
35. Aroni atavaa kanzu hiyo kutekeleza huduma yake ya ukuhani na sauti yake itasikika wakati anapoingia mahali patakatifu mbele yangu na wakati anapotoka, njuga hizo zitasikika, naye hatauawa.