4. Tuliiteka miji yake yote; hakuna hata mji mmoja ambao hatukuuteka. Jumla tuliiteka miji sitini, yaani eneo lote la Argobu ambalo lilitawaliwa na mfalme Ogu wa Bashani.
5. Miji yote hii ilikuwa na ngome zenye kuta ndefu, zilizokuwa na malango na makomeo. Kulikuwa pia na vijiji vingi ambavyo havikuzungukwa na kuta.
6. Tuliteketeza kila kitu huko, tukaharibu kila mji na kuua wanaume, wanawake na watoto kama tulivyofanya katika miji ya mfalme Sihoni wa Heshboni.
7. Lakini mifugo yote na mali tulichukua nyara.
8. “Wakati huo tuliitwaa nchi hiyo ya wale wafalme wawili wa Waamori waliokuwa wanakaa ngambo ya mto Yordani, katikati ya mto Arnoni na mlima Hermoni.
9. (Wasidoni huuita mlima huo Sirioni, nao Waamori huuita Seniri).
10. Tuliiteka miji yote katika sehemu tambarare za mwinuko, na pia eneo lote la Gileadi na Bashani mpaka Saleka na Edrei, miji ya mfalme Ogu huko Bashani.”
11. (Mfalme Ogu ndiye peke yake aliyesalia miongoni mwa Warefai. Kitanda chake kilichotengenezwa kwa chuma, kilikuwa na urefu wa mita nne na upana wa karibu mita mbili, kadiri ya vipimo vya kawaida. Kitanda hicho bado kipo katika mji wa Waamori wa Raba.)
12. “Tulipoitwaa nchi hiyo, niliwapa makabila ya Reubeni na Gadi eneo la kuanzia kaskazini mwa Aroeri karibu na Arnoni na nusu ya eneo la milima ya Gileadi, pamoja na miji yake.
13. Kisha nililipatia nusu ya lile kabila la Manase sehemu iliyobaki ya Gileadi pamoja na Bashani yote iliyotawaliwa na Ogu, yaani eneo lote la Argobu. (Nchi yote ya Bashani ilijulikana kama nchi ya Warefai.)