17. Upande wa magharibi nchi yao ilienea hadi mto Yordani, toka ziwa Galilaya upande wa kaskazini, ukashuka hadi bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, mpaka miteremko ya Pisga, upande wa mashariki.
18. “Wakati ule niliwapa maagizo haya: ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapeni nchi hii mashariki ya mto Yordani iwe mali yenu. Sasa nyinyi mashujaa kati ya ndugu zenu, chukueni silaha mvuke mto Yordani mkiwa mbele ya ndugu zenu Waisraeli.
19. Lakini wake zenu, watoto wenu na wanyama wenu, najua mnayo mifugo mingi, watabaki kwenye miji niliyowapeni.
20. Wasaidieni ndugu zenu Waisraeli mpaka Mwenyezi-Mungu atakapowajalia watulie mahali pao kama nanyi mlivyotulia, yaani nao pia waimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapatia huko ngambo ya Yordani. Baada ya hayo, mtaweza kurejea katika nchi yenu hii ambayo nimewapeni iwe yenu!’