Kumbukumbu La Sheria 29:22-29 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Katika vizazi vijavyo, wazawa wenu na wageni kutoka nchi ya mbali wataona jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoiletea nchi hii maafa na mateso:

23. Imejaa madini ya kiberiti na chumvi, imeteketea na kuwa tupu, haikupandwa mbegu na haioti chochote. Ni kama ilivyokuwa wakati Mwenyezi-Mungu alipoangamiza Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, kwa hasira yake kali.

24. Naam, mataifa yote yatasema: ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ameitendea hivyo nchi hii? Hasira hii kubwa inamaanisha nini?’

25. Na jibu litatolewa: ‘Ni kwa sababu walivunja agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao ambalo alifanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri,

26. wakaenda kuitumikia na kuiabudu miungu mingine, ambayo hawakuijua hapo awali, wala Mwenyezi-Mungu hakuwa amewapa.

27. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya nchi hii, na kuiletea laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki.

28. Naye Mwenyezi-Mungu, akawangoa kutoka katika nchi yao kwa hasira na ghadhabu kubwa, akawatupa katika nchi nyingine kama ilivyo leo.’

29. “Mambo ya siri ni ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, lakini yale ambayo ameyafunua ni yetu na wazawa wetu milele, ili tutekeleze maneno yote ya sheria hii.”

Kumbukumbu La Sheria 29