Hesabu 27:11-21 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Na ikiwa baba yake hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utakuwa wa jamaa yake wa karibu, naye ataumiliki kama mali yake. Hii itakuwa kanuni na sheria kwa Waisraeli, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu nilivyokuamuru.”

12. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Panda juu ya Mlima huu wa miinuko ya Abarimu uitazame nchi ambayo nimewapa Waisraeli.

13. Ukisha iona, nawe pia utafariki kama ndugu yako Aroni alivyofariki,

14. kwa sababu hamkuitii amri yangu kule jangwani Sini. Wakati jumuiya yote ya watu walipolalamika juu yangu kule Meriba, hamkuacha utukufu wangu uonekane mbele yao walipotaka wapewe maji.” (Meriba ni chemchemi ya maji ya Kadeshi katika jangwa la Sini).

15. Naye Mose akamwomba Mwenyezi-Mungu,

16. “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu uliye asili ya uhai wote, nakuomba umteue mtu wa kuisimamia jumuiya hii,

17. ambaye atawatangulia na kuwaongoza katika shughuli zao zote, ili wasije wakawa kama kondoo wasio na mchungaji.”

18. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mtwae Yoshua mwana wa Nuni, mtu mwenye roho nzuri, kisha umwekee mikono,

19. na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote, umkabidhi jukumu hilo.

20. Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli imtii.

21. Yeye atamtegemea kuhani Eleazari ambaye atamjulisha matakwa yangu kwa kutumia jiwe la kauli. Kwa njia hii, Eleazari atamwongoza Yoshua na jumuiya yote ya Waisraeli wanapotoka na wanapoingia.”

Hesabu 27