Hesabu 15:13-24 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Kila mwananchi Mwisraeli atafuata maagizo hayo wakati anapotoa tambiko, harufu impendezayo Mwenyezi-Mungu.

14. Na kama kuna mgeni anayeishi pamoja nanyi kwa muda au daima, akitaka kutoa sadaka yake kwa kuiteketeza, harufu impendezayo Mwenyezi-Mungu, mtu huyo atafanya kama mnavyofanya nyinyi.

15. Katika vizazi vyote vijavyo, kanuni zilezile mtakazofuata nyinyi ndizo atakazofuata mgeni yeyote atakayeishi pamoja nanyi; mbele ya Mwenyezi-Mungu mtakuwa sawa;

16. nyinyi na yeye mtakuwa chini ya sheria ileile moja na maagizo yaleyale.”

17. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waeleze

18. Waisraeli kwamba wakati watakapoingia katika nchi ninayowapeleka

19. kila mtakapokula mazao ya nchi hiyo, mtatenga kiasi fulani na kunipa mimi Mwenyezi-Mungu.

20. Mtakapooka mikate, mkate wa kwanza wa mazao ya kwanza ya nafaka yenu utatolewa kama sadaka kutoka mahali pa kupuria nafaka.

21. Mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka hii maalumu katika vizazi vyenu vyote vijavyo.

22. “Lakini ikiwa mtakosa kuzifuata amri zote ambazo mimi Mwenyezi-Mungu nimewapa kwa njia ya Mose,

23. kama siku zijazo watu hawatafuata yote ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nimemwamuru Mose,

24. basi, ikiwa kosa hilo limefanyika bila kukusudia, bila jumuiya kujua, jumuiya yote itatoa fahali mmoja mchanga kuwa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu, pamoja na sadaka yake ya nafaka na ya divai kufuatana na maagizo yake. Kadhalika watu watatoa beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi.

Hesabu 15