9. Yeshua, wanawe na jamaa yake, pamoja na Kadmieli na wanawe, (wa ukoo wa Yuda) walishirikiana kusimamia ujenzi wa nyumba ya Mungu. Walisaidiwa na wazawa wa Henadadi na ndugu zao Walawi.
10. Wajenzi walipoanza kuweka msingi wa hekalu la Mwenyezi-Mungu, makuhani wakiwa wamevalia mavazi yao rasmi, walisimama mahali pao na tarumbeta mikononi, nao Walawi wa ukoo wa Asafu wakisimama na matoazi yao; basi, walimtukuza Mwenyezi-Mungu kufuatana na maagizo ya mfalme Daudi wa Israeli.
11. Waliimba kwa kupokezana, wakimsifu na kumtukuza Mwenyezi-Mungu:“Kwa kuwa yu mwema,fadhili zake kwa Israeli zadumu milele.”Watu wote walipaza sauti kwa nguvu zao zote, wakamsifu Mwenyezi-Mungu kwa sababu ya kuanza kujengwa msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu.
12. Wengi wa makuhani, Walawi, na viongozi wa koo waliokuwa wazee na ambao walikuwa wameiona nyumba ya kwanza, walilia kwa sauti kubwa walipouona msingi wa nyumba hii mpya unawekwa, ingawa watu wengine wengi walipaza sauti kwa furaha.
13. Watu hawakuweza kutofautisha kati ya sauti za furaha na za kilio kwa sababu zilikuwa nyingi na zilisikika mbali sana.