10. Basi, mimi nikatoa unabii kama alivyoniamuru, nayo pumzi ikaingia ndani yao, nayo ikawa hai, ikasimama: Kundi kubwa ajabu.
11. Hapo Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Wewe mtu! Mifupa hiyo ni watu wote wa Israeli. Wao, wanasema, ‘Mifupa yetu imenyauka, matumaini yetu yamepotea nasi tumekwisha kabisa.’
12. Kwa hiyo, toa unabii, uwaambie, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Enyi watu wangu, nitayafunua makaburi yenu na kuwafufua kutoka makaburini mwenu. Nitawarudisha nyumbani kwenu katika nchi ya Israeli.
13. Nanyi, enyi watu wangu, mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu nitakapofunua makaburi yenu na kuwafufua kutoka makaburini mwenu.
14. Nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawaweka katika nchi yenu wenyewe. Hapo mtatambua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nimesema, nami nitafanya hayo. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
15. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia;
16. “Wewe mtu! Chukua kijiti kimoja, uandike juu yake maneno haya: ‘Kwa Yuda na Waisraeli wanaohusiana naye.’ Kisha chukua kijiti kingine, uandike juu yake maneno haya: ‘Kwa Yosefu (kijiti cha Efraimu) na Waisraeli wanaohusiana naye.’