7. Ohola alifanya zinaa na hao maofisa wote wa vyeo vya juu wa Ashuru naye akajitia unajisi kwa vinyago vyote vya kila mwanamume wake aliyemtamani.
8. Aliendelea na uzinzi wake aliouanza kule Misri wakati huo, akiwa bado kijana, wanaume walivunja ubikira wake na kuzitimiza tamaa zao kwake.
9. Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa Waashuru wapenzi wake, ambao aliwatamani sana.
10. Hao walimvua mavazi yake na kumwacha uchi. Waliwakamata watoto wake, naye mwenyewe wakamuua kwa upanga. Adhabu hiyo aliyopata ikawa fundisho kwa wanawake wengine.
11. “Oholiba dada yake, aliona jambo hilo, lakini akawa amepotoka kuliko yeye katika tamaa yake na uzinzi wake uliokuwa mbaya kuliko wa dada yake.
12. Aliwatamani sana Waashuru: Wakuu wa mikoa, makamanda, wanajeshi waliovaa sare zao za kijeshi, wapandafarasi hodari, wote wakiwa vijana wa kuvutia.
13. Nilimtambua kuwa najisi. Ama kweli wote wawili walikuwa na tabia hiyo moja.
14. Lakini Oholiba alizidisha uzinzi wake; akapendezwa na picha za Wakaldayo zilizochorwa ukutani, zimetiwa rangi nyekundu,
15. mikanda viunoni, vilemba vikubwa vichwani; hizo zote zilifanana na maofisa, naam, picha ya Wababuloni, wakazi wa nchi ya Wakaldayo.
16. Alipoziona picha hizo, mara akashikwa na tamaa, akatuma wajumbe kwenda Ukaldayo.
17. Basi, Wababuloni wakaja kulala naye. Wakamtia najisi kwa tamaa zao. Alipokwisha tiwa najisi, akajitenga nao.
18. Alipoendelea na uzinzi wake na kufunua uchi wake, mimi nilimwacha kama nilivyomwacha dada yake.
19. Hata hivyo, akazidisha uzinzi wake akifanya kama wakati wa ujana wake alipofanya uzinzi kule Misri.