Ezekieli 21:4-10 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Tangu kaskazini hadi kusini, nitawakatilia mbali watu wote, wema na wabaya, kwa upanga wangu.

5. Watu wote watajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndiye niliyeuchomoa upanga alani mwake na wala hautarudishwa tena ndani.

6. “Nawe mtu, jikunje kama mtu aliyekata tamaa, uomboleze mbele yao.

7. Wakikuuliza, ‘Kwa nini unaomboleza?’ Utawaambia: ‘Naomboleza kwa sababu ya habari zinazokuja.’ Kila mtu atakufa moyo, mikono yao yote italegea; kila aishiye atazimia na magoti yao yatakuwa kama maji. Habari hizo zaja kweli, nazo zinatekelezwa. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”

8. Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

9. “Wewe mtu, toa unabii useme: Mwenyezi-Mungu asema hivi:Upanga! Naam, upanga umenolewa,nao umengarishwa pia.

10. Umenolewa ili ufanye mauaji,umengarishwa umetamete kama umeme!

Ezekieli 21