7. Mfalme akasimama kwa hasira, akatoka chumbani kwenye karamu ya divai na kwenda nje kwenye bustani ya ikulu. Hamani alipoona kwamba mfalme amenuia kumwadhibu, alibaki nyuma kumsihi malkia Esta ayasalimishe maisha yake.
8. Baadaye mfalme alirudi kutoka bustanini, na mara alipoingia chumbani walimokuwa wanakunywa divai, alimkuta Hamani amejitupa karibu na kochi ambamo Esta alikuwa amekaa. Kuona hivyo, mfalme alisema kwa sauti kuu, “Hivi mtu huyu anataka kumshika kwa nguvu malkia mbele yangu, tena ndani ya ikulu?” Mara kabla mfalme hajamaliza kusema, matowashi wakamfunika Hamani uso.
9. Harbona, mmoja wa wale matowashi waliomhudumia mfalme, akasema, “Hamani amethubutu hata kutengeneza mti wa kumwulia Mordekai ambaye aliyaokoa maisha yako, ewe mfalme. Mti huo, wenye urefu wa mita ishirini na mbili, bado uko huko nyumbani kwake.” Hapo mfalme akaamuru, “Mwulie Hamani papo hapo.”
10. Naye, Hamani akauawa hapo kwenye mti wa kuulia aliokuwa amemtayarishia Mordekai. Basi, hasira ya mfalme ikapoa.