1. “Katika mwaka Dario mwana wa Ahasuero, Mmedi, alipoanza kutawala juu ya milki ya Wakaldayo,
2. mimi Danieli nilikuwa nikivisoma kwa makini vitabu vitakatifu, na humo nikaelewa maana ya jambo lile Mwenyezi-Mungu alilomfahamisha nabii Yeremia kuhusu ile miaka sabini, muda ambao utahusika na kuharibiwa kwa Yerusalemu.
3. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, kwa moyo, nikimtolea dua pamoja na kufunga, nikavaa vazi la gunia na kuketi kwenye majivu.
4. Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, na kuungama, nikisema:“Ee Bwana, wewe ni Mungu mkuu na wa kuogofya. Wewe ni mwaminifu kwa agano lako na unawafadhili wakupendao na kuzitii amri zako.
5. Tumetenda dhambi, tumekosa, tumetenda maovu na kukuasi. Tumezikiuka amri zako na kanuni zako.