11. Walimchinja mwanakondoo wa Pasaka, nao makuhani walinyunyiza damu, waliyopokea kutoka kwao nao Walawi waliwachuna wanyama.
12. Halafu walitenga sadaka za kuteketeza ili waweze kuzigawa kulingana na jamaa zao walio makuhani ili wamtolee Mwenyezi-Mungu kama ilivyoandikwa katika kitabu cha Mose. Nayo mafahali waliwafanya vivyo hivyo.
13. Walimchoma mwanakondoo wa Pasaka juu ya moto kama ilivyoagizwa, na pia walizitokosa sadaka takatifu katika vyungu, masufuria na kwenye vikaango, na kuwagawia upesiupesi watu wasiofanya kazi ya ukuhani.
14. Baadaye, Walawi wakajiandalia sehemu zao na za makuhani kwa maana makuhani wa uzao wa Aroni walikuwa wanashughulika na utoaji wa sadaka za kuteketeza, na vipande vya mafuta, mpaka usiku; kwa hiyo Walawi waliandaa kwa ajili yao wenyewe na kwa ajili ya makuhani wa uzao wa Aroni.
15. Nao waimbaji wazawa wa Asafu walishika nafasi zao, kwa mujibu wa maagizo ya mfalme Daudi, Asafu, Hemani na Yeduthuni, mwonaji wa mfalme. Nao mabawabu walikuwa kwenye malango; hawakuhitajika kuziacha nafasi zao za kazi kwa kuwa ndugu zao Walawi waliwaandalia Pasaka.