2 Mambo Ya Nyakati 33:11-17 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu akawaleta makamanda wa jeshi la mfalme wa Ashuru. Hao makamanda walimkamata Manase kwa kulabu wakamfunga pingu za shaba, wakampeleka hadi Babuloni.

12. Wakati alipokuwa taabuni, alimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akajinyenyekesha sana mbele ya Mungu wa babu zake.

13. Alimsihi, naye Mungu akapokea ombi lake na sala yake akamrudisha Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu.

14. Baada ya haya, Manase alijenga ukuta mwingine upande wa nje wa mji wa Daudi, magharibi mwa Gihoni, bondeni, akauendeleza hadi Lango la Samaki, akauzungusha hadi Ofeli; akauinua juu sana. Pamoja na hayo, aliweka makamanda wa majeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome.

15. Alitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu miungu yote ya kigeni na sanamu pamoja na madhabahu zote alizokuwa amezijenga kwenye mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika Yerusalemu; alivitupa nje ya mji.

16. Alirudisha madhabahu ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, na juu yake akatoa tambiko za amani na za shukrani, akawaamuru watu wa Yuda wamwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

17. Hata hivyo watu waliendelea kutoa sadaka mahali pa kufanyia ibada, lakini kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao tu.

2 Mambo Ya Nyakati 33