4. Je, hatuna haki ya kula na kunywa?
5. Je, hatuna ruhusa kumchukua mke Mkristo katika ziara zetu, kama vile wafanyavyo mitume wengine, ndugu zake Bwana, na pia Kefa?
6. Au ni mimi tu na Barnaba ambao tunapaswa kujipatia maslahi yetu kwa kufanya kazi?
7. Je, mwanajeshi gani anayelipia utumishi wake jeshini? Mkulima gani asiyekula matunda ya shamba lake la mizabibu? Mchungaji gani asiyekunywa maziwa ya mifugo yake?
8. Je, nasema mambo haya kibinadamu tu? Je, sheria nayo haisemi hivyo?
9. Imeandikwa katika sheria: “Usimfunge kinywa ng'ombe anapopura nafaka.” Je, ndio kusema Mungu anajishughulisha na ng'ombe?