27. Hiramu pia alitengeneza magari kumi ya shaba, kila gari likiwa na urefu wa mita 1.75, upana wa mita 1.75, na kimo cha mita 1.25.
28. Magari hayo yalikuwa yameundwa hivi: Kulikuwa na mabamba ya chuma ambayo yalikuwa yameshikiliwa na mitalimbo. Juu ya mabamba hayo yaliyoshikiliwa na mitalimbo,
29. kulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe wenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali, zilikuwa zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuri.
30. Isitoshe, kila gari lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya katikati vya kuyazungukia magurudumu hayo, vilikuwa vya shaba. Kwenye pembe nne za gari kulikuwa na vishikizo vya shaba kwa ajili ya birika kubwa. Karibu ya kila kishikio kuliwekwa mapambo ya maua ya kusokotwa.
31. Mlango wa gari ulikuwa katika sehemu iliyotokeza juu kwa kiasi cha nusu mita. Kwa nje, mlango ulikuwa umetiwa michoro; na mabamba yake yalikuwa ya mraba, si ya mviringo.
32. Na hayo magurudumu manne yalikuwa chini ya yale mabamba; vyuma vya katikati kuzunguka magurudumu hayo vilikuwa vimeunganishwa na mfumo wa gari lenyewe; na kimo cha magurudumu hayo kilikuwa sentimita 66.