11. Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Waaramu na kuwaangamiza.’”
12. Hata wale manabii wengine wote wakatabiri vivyo hivyo, wakasema, “Nenda uushambulie Ramoth-gileadi, utashinda! Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.”
13. Wakati huo, yule mtumishi aliyetumwa kwenda kwa Mikaya, alimwambia, “Manabii wengine wote kwa pamoja, wamemtabiria mfalme ushindi; tafadhali, nawe pia ufanye kama wao, umtabirie mema.”
14. Lakini Mikaya akamjibu, “Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, mimi nitasema tu yale atakayoniambia Mwenyezi-Mungu.”
15. Basi, Mikaya alipofika mbele ya mfalme, mfalme alimwuliza, “Je, twende kupigana vita huko Ramoth-gileadi ama tusiende?” Naye alimjibu, “Nenda na ufanikiwe, naye Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.”
16. Lakini mfalme akamwambia, “Nitakuapisha mara ngapi kwamba unaposema nami kwa jina la Mwenyezi-Mungu, ni lazima uniambie ukweli mtupu?”
17. Ndipo, Mikaya akasema, “Niliona watu wote wa Israeli wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji. Naye Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi; basi warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.’”
18. Hapo, mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kamwe hatatabiri jema juu yangu ila mabaya tu?”