24. Kisha, wao watamwomba mungu wao, nami nitamwomba Mwenyezi-Mungu. Mungu atakayejibu kwa kuleta moto, huyo ndiye Mungu wa kweli.” Na hapo umati wote ukasema, “Naam! Na iwe hivyo.”
25. Kisha, Elia akawaambia manabii wa Baali, “Nyinyi ni wengi; basi anzeni. Jichagulieni fahali, mtayarisheni na kumwomba mungu wenu, lakini msiwashe moto.”
26. Hao manabii wakamtwaa fahali wao waliyepewa, wakamtayarisha, kisha wakaanza kumlilia Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakirukaruka na kuyumbayumba kuizunguka madhabahu waliyotengeneza wakisema: “Ee Baali, utusikie!” Lakini hapakutokea sauti yoyote, wala hakuna aliyewajibu.
27. Ilipofika saa sita mchana, Elia akaanza kuwadhihaki akisema, “Ombeni kwa sauti kubwa zaidi! Yeye ni mungu ati! Huenda ikawa amezama katika mawazo yake, amekwenda haja, au yumo safarini! Labda amelala, mnapaswa kumwamsha!”