1 Wafalme 11:26-31 Biblia Habari Njema (BHN)

26. Yeroboamu mwana wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumishi wa Solomoni, ambaye mama yake mjane, aliitwa Zerua, pia alimwasi mfalme.

27. Kisa cha uasi huo ni hiki: Solomoni alipokuwa akishughulika na kusawazisha sehemu ya Milo, na kuimarisha kuta za mji wa baba yake Daudi,

28. Yeroboamu alionekana kuwa kijana hodari na shujaa. Ndipo Solomoni alipoona kwamba huyo kijana alikuwa mwenye bidii, akamweka awe msimamizi wa kazi za kulazimishwa zilizofanywa na watu wa ukoo wa Yosefu.

29. Siku moja, Yeroboamu alipokuwa akisafiri kutoka Yerusalemu, nabii Ahiya wa Shilo alikutana naye njiani. Ahiya alikuwa amevaa vazi jipya. Wote wawili walikuwa peke yao mashambani.

30. Mara, Ahiya akalivua vazi lake jipya, akalirarua vipande kumi na viwili,

31. halafu akamwambia Yeroboamu, “Jitwalie vipande kumi maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Tazama, karibu nitaurarua ufalme na kuuondoa mikononi mwa Solomoni, nami nitakupa wewe makabila kumi.’

1 Wafalme 11