4. Hivyo, walituma watumishi huko Shilo, nao wakalileta sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu wa majeshi ambaye anakaa kifalme juu ya viumbe wenye mabawa. Wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi walikuja pamoja na lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.
5. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipofika kambini Waisraeli wote walishangilia kwa furaha, hata nchi yote ikatikisika.
6. Wafilisti waliposikia sauti hiyo ya furaha walisema “Kelele hizo zote kambini mwa Waebrania zina maana gani?” Walipojua kwamba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilikuwa limewasili kambini mwa Waisraeli,
7. Wafilisti waliogopa; wakasema, “Bila shaka, miungu imewasili kambini mwao! Ole wetu! Jambo kama hili halijawahi kutokea.
8. Ole wetu! Ni nani atakayeweza kutuokoa kutokana na miungu hiyo yenye nguvu? Hiyo ni miungu iliyowaua Wamisri kwa kila aina ya mapigo jangwani.
9. Sasa, enyi Wafilisti, jipeni moyo. Muwe, hodari msije mkawa watumwa wa Waebrania kama wao walivyokuwa watumwa wetu. Muwe hodari kama wanaume na kupigana.”
10. Wafilisti walipiga vita, na Waisraeli walishindwa na kukimbia kila mtu nyumbani kwake. Siku hiyo kulikuwa na mauaji makubwa kwani askari wa miguu 30,000 wa Israeli waliuawa.