15. Nathani alimwelezea Daudi mambo yote haya kulingana na maono yote.
16. Kisha mfalme Daudi akaingia ndani ya hema na kuketi mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu akaomba, “Mimi ni nani, ee Mwenyezi-Mungu, na nyumba yangu ni nini hata unitukuze hivi?
17. Isitoshe, umenifanyia mengine zaidi: Umenitolea ahadi juu ya vizazi vyangu vijavyo ee Mwenyezi-Mungu!
18. Nikuambie nini zaidi, mimi Daudi mtumishi wako, kwa kunitukuza hivyo? Wewe unanijua mimi mtumishi wako.
19. Ee Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya mtumishi wako na kwa kufuatana na moyo wako mwenyewe, umeyatenda hayo makuu yote, ili yajulikane hayo matendo makuu yote.
20. Hakuna mwingine kama wewe, ee Mwenyezi-Mungu, na yote tunayoyasikia yanathibitisha kwamba hakuna Mungu mwingine ila wewe.